Mwanamke Aingiziwa chupa sehemu za siri na kushambuliwa kwa waya za umeme

Mkazi wa Kitangiri jijini Mwanza, Biera Edwin (22) amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya jiji  Sekou Toure akipatiwa matibabu baada ya kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake kwa tuhuma za kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mume wa mtu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola hakupatikana kuzungumzia tukio hilo, lakini Biera mwenyewe alisema kabla ya kufanyiwa kitendo hicho mama ambaye ni jirani yao
alimtuma mtoto wake amwite nyumbani kwao, alipokwenda mama huyo alianza kumshambulia.
Alisema alimshambulia akishirikiana na marafiki zake na kumjeruhi vibaya kwa nyaya za umeme, kumwingizia chupa kwenye sehemu zake za siri na baadaye kuchoma nguo zake.

Binti huyu kwa sasa amelazwa katika wadi ya majeruhi kwenye Hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure akipatiwa matibabu na alisema baada ya kufanyiwa ukatili huo pia waliteketeza nguo zake kwa moto.





Kamanda wa polisi mkoa wa mwanza,Valentino mlowola

Naye dada wa majeruhi, Nice Cosmas anaeleza kuwa akiwa nyumbani kwao, mama huyo wa jirani alituma watoto wake ambao walieleza kuwa wakamchukue mtu wao.
Alisema walipokwenda hapo jirani alimkuta ndugu yake akiwa hana nguo huku akiwa amejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake.

Alisema walilazimika kurudi nyumbani kumchukulia nguo za kumvisha na kisha kutoa taarifa kwa mamlaka husika kabla ya kumpeleka hospitali kwa matibabu.

Baadhi ya viongozi wa mtaa wa Kitangiri A walisikitishwa na kitendo hicho na kuomba vyombo vya sheria kuwachukulia hatua kali wahusika.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kitangiri A, Issa Salum alisema wanataka haki itendeke kwani kitendo hicho ni nusu ya mauaji.

Naye Mjumbe wa Serikali za Mitaa, Mariam Yusuf alisema mama huyo wa jirani alipaswa kutoa taarifa kwa mabalozi ama kwa wazazi wa binti huyo kama alikuwa na uhakika na madai yake kabla ya kuchukua ukatili dhidi ya binti huyo.